Friday, October 24, 2014

BASATA KUMVUA TAJI MISS TANZANIA


BASATA Kumvua Taji Miss Tanzania 2014 Kwa
Kudanganya Umri
Sakata la lililojitokeza la mrembo wa Taifa wa
mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2014', Sitti
Mtemvu kudaiwa kudanganya umri, limeingia
katika sura mpya baada ya Baraza la Sanaa
Tanzania (Basata) kueleza kuwa litamvua taji
hilo endapo itabainika kweli alichakachua umri
wake.
Katibu Mkuu wa Basata, Geoffrey Mwingereza,
aliliambia NIPASHE jana kuwa baraza hilo
linasubiri uchunguzi ukamilike na endapo
watabaini kuna udanganyifu ulifanyika
hawatakuwa na la kufanya zaidi ya kumvua taji.
Wakati Mwingereza akieleza hayo, viongozi wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo wanatarajia kukutana leo jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kujadili sakata hilo la Sitti.
Akizungumza na NIPASHE jana, Naibu Waziri wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Juma Nkamia, alisema serikali
imesikia taarifa za mkanganyiko kuhusiana na
mrembo huyo hivyo imeamua kuitisha kikao ili
kuanza kulifanyia kazi.
Nkamia alisema kamwe serikali
haiwezi kukaa kimya pale ambapo
jina la nchi linatajwa vibaya.
"Siwezi kukuambia hatua gani
zitachukuliwa, ila kesho (leo)
tutakuwa na kikao, serikali haiwezi
kukaa kimya, kuna vyombo vyake
vinalifanyia kazi," alisema Naibu
Waziri huyo.
Aliongeza kuwa yeye alikuwa nje
ya Dar es Salaam, lakini tayari
kuna maelekezo aliyoyatoa na
yameanza kufanyiwa kazi na
wizara hiyo.
Siku moja baada ya Sitti
kutangazwa mshindi wa taji hilo,
taarifa za mrembo huyo kuhusu umri wake
zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii
zikionyesha kuwa ana miaka 25, hivyo hana sifa
za kushiriki shindano hilo hapa nchini.
Nakala ya hati ya kusafiria ya mrembo huyo
ambayo ilitolewa Februari 15, 2007 na muda
wake wa kumaliza kutumika ukiwa ni Februari
14, 2017 yenye namba AB 202696 inaonesha
Sitti ambaye pia anashikilia taji la Kitongoji cha
Chang'ombe na Kanda ya Temeke, alizaliwa
Mei 31, 1989.Pia taarifa nyingine zinazoone sha
mrembo huyo ana miaka 25 ni zilizokuwa
kwenye Taasisi ya Explore Talent, ikimtaja
kwamba anaishi Dallas, Texas, urefu wake ni
5'8, umbo lake ni la kati, asili yake ni Mwafrika
na rangi ya macho yake ni kahawia.
Juzi, Kamati ya Miss Tanzania iliyoko chini ya
Mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga,
ilisema kuwa Sitti amezaliwa Mei 31, 1991 katika
wilaya ya Temeke jijini kwa mujibu wa cheti
chake cha kuzaliwa alichokionesha.
Lundenga alionesha cheti cha kuzaliwa cha Sitti
ambacho kimetolewa na Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA) Septemba 9, mwaka
huu kikiwa na namba 1000580309 na kikimtaja
baba yake ni Abbas Mtemvu Zuberi (Mbunge-
Temeke) wakati mama ni Mariam Nassor Juma
(Diwani- Temeke).
Hata hivyo, Lundenga alisema kuwa kamati
yake inaendelea na uchunguzi kuhusiana na
taarifa hizo na endapo watabaini kuwepo na
udanganyifu watamchukulia hatua mrembo
huyo kwa kushirikiana na Basata.
Pia Lundenga na Sitti, walikanusha taarifa za
mrembo kuwa kuwa na mtoto na kusema
kwamba mwenye uthibitisho wa jambo hilo
anatakiwa aliwasilishe kwa kamati ili hatua
zichukuliwe.
Sitti aliibuka kidedea katika shindano la urembo
la taifa lililofanyika usiku wa Jumamosi ya
Oktoba 11 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini
na kuwashinda washiriki wenzake 29 waliokuwa
wanawania taji hilo.

No comments:

Post a Comment